Wednesday, December 30, 2009

Iran yashutumu mataifa ya magharibi kwa ghasia.


Mwakilishi wa kiongozi mkuu wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema jana kuwa viongozi wa upinzani ni maadui wa Mwenyezi Mungu, ambao wanastahili kuuwawa kwa mujibu wa sheria ya dini ya Kiislamu ya Sharia.

Taarifa hiyo iliyotolewa na kiongozi wa kidini Abbas Vaez-Tabasi imeingiliana na maandamano ya mamia kwa maelfu ya waungaji mkono Serikali ambao walikuwa wakitoa wito kwa viongozi wa upinzani kuadhibiwa kwa kuchochea ghasia baada ya uchaguzi wa rais mwezi Juni.

Matamshi ya Vaez-Tabasi yamekuja siku mbili baada ya watu wanane kuuwawa katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyotokana na uchaguzi uliobishaniwa wa Juni mwaka huu ambapo rais aliyeko madarakani mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmedinejad alishinda.

Vurugu za kisiasa zimeingia katika awamu mpya nchini Iran kukiwa na mapambano yaliyomwaga damu pamoja na kukamatwa kwa wapinzani , huku majeshi ya usalama yakitoa wito kwa maafisa kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa upinzani.

Kiasi watu maarufu 20 kutoka upande wa upinzani wamekamatwa tangu siku ya Jumapili, ikiwa ni pamoja na washauri waandamizi wa kiongozi wa upinzani Mir Hossein Moussavi, shemeji yake pamoja na dada yake mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Shirin Ebadi, imeeleza tovuti ya upinzani.

No comments:

Post a Comment